Exodus 20

Amri Kumi

(Kumbukumbu 5:1-21)

1 aNdipo Mungu akasema maneno haya yote:

2 b“Mimi ndimi Bwana Mwenyezi Mungu wako, niliyekutoa Misri, kutoka nchi ya utumwa.
3 cUsiwe na miungu mingine ila mimi.
4 dUsijitengenezee sanamu katika umbo la kitu chochote kilicho juu mbinguni, au duniani chini, au ndani ya maji. 5 eUsivisujudie wala kuviabudu; kwa kuwa Mimi, Bwana Mwenyezi Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu, ninayewaadhibu watoto kwa ajili ya dhambi za baba zao hadi kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, 6 flakini ninaonyesha upendo kwa maelfu ya vizazi vya wale wanipendao na kuzishika amri zangu.
7 gUsilitaje bure jina la Bwana Mwenyezi Mungu wako, kwa kuwa Bwana hataacha kumhesabia hatia yeye alitajaye jina lake bure.
8 hIkumbuke siku ya Sabato, uitakase. 9 iKwa siku sita utafanya kazi na kutenda shughuli zako zote, 10 jlakini siku ya saba ni Sabato kwa Bwana Mwenyezi Mungu wako. Siku hiyo hutafanya kazi yoyote, wewe, wala mwanao au binti yako, wala mtumishi wako wa kiume au wa kike, wala wanyama wako, wala mgeni aliye ndani ya malango yako. 11 kKwa kuwa kwa siku sita, Bwana aliumba mbingu na nchi, bahari na vyote vilivyomo, lakini akapumzika siku ya saba. Kwa hiyo Bwana akaibariki siku ya Sabato na kuifanya takatifu.
12 lWaheshimu baba yako na mama yako, ili upate kuishi siku nyingi katika nchi anayokupa Bwana Mwenyezi Mungu wako.
13 mUsiue.
14 nUsizini.
15 oUsiibe.
16 pUsimshuhudie jirani yako uongo.

17 qUsiitamani nyumba ya jirani yako. Usimtamani mke wa jirani yako, wala mtumishi wake wa kiume au wa kike, wala ng’ombe wake au punda wake, wala chochote kile alicho nacho jirani yako.”

Watu Wanaogopa

(Kumbukumbu 5:22-33)

18 rWatu walipoona ngurumo na radi, na kusikia mlio wa tarumbeta, na kuuona mlima katika moshi, walitetemeka kwa woga. Wakasimama mbali 19 sna wakamwambia Musa, “Sema nasi wewe mwenyewe, nasi tutakusikiliza. Lakini usimwache Mungu aseme nasi, la sivyo tutakufa.”

20 tMusa akawaambia watu, “Msiogope! Mungu amekuja kuwajaribu, ili kwamba hofu ya Mungu iwakalie, msitende dhambi.”

21 uWatu wakabaki mbali, wakati Musa alipolisogelea lile giza nene mahali pale Mungu alipokuwa.

Sanamu Na Madhabahu

22 vKisha Bwana akamwambia Musa, “Waambie Waisraeli hivi: ‘Mmejionea wenyewe kwamba nimesema nanyi kutoka mbinguni: 23 wMsijifanyizie miungu yoyote na kuilinganisha nami, msijitengenezee miungu ya fedha wala miungu ya dhahabu.

24 x“ ‘Utanitengenezea madhabahu ya udongo, na juu yake utoe sadaka za kuteketezwa kwa moto na sadaka za amani, kondoo zako, mbuzi na ng’ombe zako. Popote nitakapofanya Jina langu liheshimiwe, nitakuja kwenu na kuwabariki. 25 yIkiwa unanitengenezea madhabahu ya mawe, usiijenge kwa mawe ya kuchonga, maana mkitumia chombo cha kuchongea mtaitia unajisi. 26 zMsitumie ngazi kupandia kwenye madhabahu yangu, uchi wako usije ukadhihirika kwa chini.’
Copyright information for SwhKC